Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Filamu ya Mu'awiya ni simulizi ambayo inaonekana kama vile imeandikwa na Mu'awiya mwenyewe kwa ajili ya kuipotosha historia. Katika kazi hii, taswira ya ukoo wa Abu Sufyan imesafishwa kiasi kwamba inaonesha hawakuwahi kuwa na uadui na Mtume (s.a.w.), Mu'awiya ameonyeshwa kama mtu mwenye busara, mwanasiasa mahiri na kiongozi makini ambaye hakuwahi kufanya makosa yoyote maishani mwake, huku sura yake halisi na matendo yake maovu ya kihistoria yakifichwa.
Filamu hii haizungumzii kabisa nafasi ya Mu'awiya katika kudhoofisha ukhalifa wa Imam Ali (a.s.), hila alizotumia katika kufanya suluhu na Imam Hasan (a.s.), wala msingi wa kuanzisha utawala wa kurithishana madaraka. Vilevile, haielezi maovu aliyowatendea maswahaba wa Mtume (s.a.w.) wala dhuluma zake dhidi ya wapinzani wake. Simulizi hii yenye upendeleo inamchora Mu'awiya kwa taswira iliyopotoshwa kabisa, isiyolingana na vyanzo vya kihistoria vyenye kuaminika.
Moja ya dosari kubwa katika filamu hii ni kuondoshwa makusudi sehemu muhimu za historia ambazo zingeeleza sura halisi ya Mu'awiya. Matukio muhimu ambayo yangetoa picha ya kweli kumuhusu yeye, ama yameondolewa au kupotoshwa ili kumwonyesha Mu'awiya kama mtu mtetezi wa amani na asiye na makosa, wakati ambapo vyanzo vya kihistoria vinaelezea tofauti kabisa kuhusiana na tabia yake.
Kwa mfano, filamu hiyo haitoi maelezo yoyote kuhusu njama za Mu'awiya dhidi ya utawala wa Imam Ali (a.s). Vita vya Siffin, ambavyo ni mojawapo ya matukio muhimu zaidi katika historia ya Uislamu, vilivyomalizika kutokana na hila zake, na kwa manufaa yake vita ambavyo vilileta tofauti katika umma wa Kiislamu. Aidha, baada ya kupata madaraka, Mu'awiya alikiuka ahadi za mkataba wa amani na Imam Hasan (a.s), na badala yake alianzisha ukandamizaji dhidi ya Shi'a na kubadilisha utawala wa Umaiyyah kuwa mfumo wa kifalme wenye kurithishana.
Miongoni mwa nukta nyengine zilizoachwa katika filamu, ni tabia ya ukatili aliyokuwa nayo Muawiya dhidi ya maswahaba wa Mtume (s.a.w). Wafuasi wengi waaminifu wa Mtume, kama vile Ammar bin Yasir na Hujir bin Adi, walipata shahada au kuteswa kwa amri yake. Hata hivyo, filamu hiyo inamwonyesha Muawiya kama mtu mvumilivu na mzungumzaji mzuri, wakati ambapo historia inathibitisha kuwa alitumia kila aina ya ukatili ili kubakisha utawala wake.
Vile vile, sera zake za kiuchumi ambazo zilisababisha kuenea kwa matabaka katika jamii, ufisadi na ubaguzi mkubwa. Muawiya alikubali kutoa hongo zisizo na kipimo na aliingiza utamaduni wa kifahari katika utawala wa kiislamu. Hata hivyo, filamu inamwonyesha kama mtawala mwenye busara ambaye alikuwa akitafuta umoja na amani kwa waislamu.
Kwa upande mwingine, filamu hii inazingatia maisha ya Muawiya pekee, na kupuuzia mbali kabisa wahusika waliokuwa wapinzani wake, na kuisimulia historia kwa mtindo wa upendeleo, kazi hii siyo uwakilishi wa haki, bali ni juhudi wazi za kuonyesha picha ya kipekee ya familia ya Banu Umayya; picha ambayo hata Wafalme wa Umayya walitamani historia iwaandike hivyo. Upotoshaji huu wa makusudi umekuwa ni njia ya kubadili filamu kutoka kuwa hadithi ya kihistoria na hatimae kuwa chombo cha upotoshaji wa historia.
Nukta nyengine ni ubora wa chini uliopo kwenye filamu hii ukilinganisha na bajeti kubwa iliyotumika, kwa kuzingatia gharama kubwa za utengenezaji, ilitarajiwa kuwa ingekuwa na drama yenye nguvu, uongozi wa kitaalamu, na uigizaji bora, lakini matokeo yake imekuwa ni filamu ya kawaida na dhaifu ambayo hata haikuweza kuwavutia wachambuzi.
Katika mtazamo wa kisiasa, wataalamu wanaitakidi kuwa filamu ya "Maawiya" ni zaidi ya kazi ya kihistoria na inafuata malengo ya kisasa. Mohammed bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia kwa msaada wa mradi huu, anataka kuhalalisha mambo yake kwa kuiga sera za Maawiya, anataka kuleta mabadiliko yake yanayozua mjadala na kuonyesha sura mpya ya utawala wa Saudi Arabia.
Kama vile ambavyo Muawiya alivyogeuza Khilafa kuwa utawala wa kifalme na urithi, Mohamed bin Salman pia anajaribu kubadilisha muundo wa utawala wa Saudi Arabia. Kusafisha sura ya Muawiya katika filamu hii kunaweza kuwa juhudi za kuhalalisha sera za bin Salman na kuimarisha mamlaka yake, kazi hii si tu kwamba imepotoka na historia, bali pia imekuwa chombo cha kutekeleza malengo ya kisiasa.
Hakuna shaka kwamba filamu ya «Maawiya» haiwezi kuonekana kama simulizi ya kihistoria pekee, bali inapaswa kuonekana kama mradi wa nyanja nyingi unaochangia katika upotoshaji wa historia huku ukihudumia malengo ya kisiasa ya leo.
Muhammad Jawad Khamsa
Maoni yako